Watu wengi hapa nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la
kujipatia chakula na kipato. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni
pamoja na mayai, nyama, mbolea na manyoya kwa matumizi mbalimbali.
Mifumo ya ufugaji kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria
na shadidi. Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa kufuata
kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
• Kufuga kuku kwenye banda bora,
• Kuchagua kuku bora wa kufuga,
• Kutunza na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
• Kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuku
• Kutunza kumbukumbu.
1 Banda la Kuku
Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Banda
bonda la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
• Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya
hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja
na wanyama hatari,
• Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi
kufanyika kwa urahisi,
• Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo
mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu,
• Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala
• Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na
sehemu ya kulelea vifaranga,
• Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka
vyombo vya chakula na maji,
• Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu
ya kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa
• Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu
unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili
kupitishia hewa na mwanga.
1.1 Vifaa Vinavyotumika kwa Ujenzi wa Banda
Vifaa vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake
katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
• Sakafu - Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
• Kuta - Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi, udongo, matofali,
mawe, mabati na wavu
• Paa - Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
• Wigo - Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi,matete,
wavu na mabati
1.2 Ukubwa wa Banda
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la
kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina na njia
ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16
wa umri wa wiki 1 – 4. Hivyo banda lenye mita za mradi 16
linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki 4. Baada ya wiki 4 eneo
hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na njia inayotumika katika
ufugaji kama inavyoonekana kwenye jedwali Na. 10
Jedwali Na 10: Eneo Linalohitajika Kufuga Kuku Kwenye
Sakafu ya Matandazo Kutegemea na Umri na Aina ya Kuku
Umri wa Kuku Idadi ya Kuku kwa mita 1 ya mraba
Kuku wa mayai Kuku wa nyama
Siku 1 hadi wiki 4 18 18
Wiki ya 5 hadi ya 8 9 9
Wiki ya 9 hadi 20 6 -
Wiki 21 kuendelea 3-4 -
Angalizo:
Mabanda yanayozungushiwa wigo kama ilivyo katika mfumo wa nusu
huria, kuku mmoja huhitaji eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba
10. Mfano, kuku 100 huhitaji eneo la mita za mraba 1000
1.3 Vifaa na Vyombo Muhimu
Mfugaji anashauriwa kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na
kuboresha utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku. Vifaa na vyombo
vinavyohitajika kwa ajili ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na
kupumzika vinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za mifugo. Aidha,
mfugaji anaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zilizopo
kwenye mazingira yake.
2 Uchaguzi wa Kuku Bora wa KuAfuga
2.1 Kuku wa Asili
Aina za kuku wa asili wanaopatikana hapa nchini ni pamaja na Kuchi
(Kuza), pori (Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji).
Mfugaji anaweza kuongeza uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa
zifuatazo:-
• Uwezo wa kutaga mayai mengi (kati ya 15-200 katika mzunguko
mmoja wa utagaji (Jedwali Na 11),
• Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi,
• Uwezo wa kustahimili magonjwa
• Umbo kubwa na kukua haraka.
Jedwali Na 11: Masuala ya Kuzingatia Wakati wa Kumchagua Kuku
Mtagaji Asili
Viungo vya mwili Sifa
Macho Maangavu, yenye wekundu kwa mbali na
makubwa yamejaa kwenye soketi za
macho.
Mdomo Wenye rangi ya njano kwa mbali
Kisunzu/Upanga Chekundu, Laini,kimelala kidogo upande
na kinang’aa
Shingo Iliyosimama
Umbali kati ya kidali
na nyonga
Upanga wa vidole 3-4 vya mpimaji
Upanga wa nyonga Upana wa vidole 3 vya mpimaji
2.2 Kuku wa Kisasa
Kuku bora wa kisasa kwa ajili ya mayai au nyama ni mwenye sifa
zifuatazo:-
• Uwezo wa kuanza kutaga wakiwa na umri mdogo (miezi 5-6)
kutegemea na koo,
• Umbo kubwa na anayekula haraka (kilo 1.5-2.0 kwa kipindi cha
wiki 8-120 kutegemea na koo kwa kuku wa nyama,
• Anayetaga mayai mengi (250 au zaidi) kwa kuku wa mayai kwa
mwaka; na
• Awe na uwezo wa kutaga katika umri wa miezi 6-8.
2.3 Uchaguzi wa Jogoo Bora wa Mbegu
Jogoo wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:-
• Achaguliwe kutoka kwenye koo zenye sifa ya kutaga mayai
mengi,
• Mrefu, umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu,
• Awe machachari, ushawishi kwa mitetea na ari ya kupanda
• Uwezo wa kupanda akiwa na umri wa miezi 7-10.
3 Mayai kwa Ajili ya Kutotoa Vifaranga
3.1 Uchaguzi wa Mayai
Mayai kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
• Yaliyorutubishwa na jogoo,
• Yasiwe na nyufa,
• Yasiwe na maganda tepetepe,
• Yasiwe na kiini kilichovunjika,
• Yawe na ukubwa wa wastani; na
• Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2 baada ya kutagwa.
3.2 Utunzaji wa Mayai
Mayai ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa
kusimamishwa wima sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku
3 za mwanzo na kisha yageuzwe ili sehemu iliyobutu iangalie chini. Mayai
yahifadhiwe kwenye sehemu iliyo na ubaridi kidogo na giza.
4. Utunzaji wa Kuku kwa Makundi
1. Utunzaji wa Vifaranga
Malezi bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu
vifaranga hawana uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara
wanapoanguliwa.Ukosefu wa malezi bora husababisha vifaranga kuwa
dhaifu,kufa kwa wingi na hivyo kupunguza idadi ya kuku wa baadaye.
Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa kutumia kuku walezi au
kutumia vifaa maalum.
Kulea Vifaranga kwa Kutumia Kuku Mlezi
Vifaranga wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku
wengi wametotoa vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi
aliye na uwezo wa kulea vifaranga wengi kati ya waliototoa aendelee kulea
na wengine waliototoa waachwe huru ili warudi kwenye mzunguko wa
kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga 20 hadi 25. Mfugaji wa
kuku,pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia yafuatayo:-
• Kuku anayelea vifaranga atengewe chumba maalumu, apewe maji ya
kutosha na chakula chenye virutubisho muhimu,
• Vifaranga wasiachiwe kutoka nje hadi watakapofika umri wa wiki 6,
• Vifaranga watengwe na mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama
aendelee na mzunguko wa kutaga;na
• Katika maeneo yenye hali ya hewa ya ubaridi vifaranga
wacheleweshwe kutenganishwa na mama/mlezi hadi wiki ya 6 au
mpaka waonekane wameota manyoya ya kutosha
Kulea Vifaranga kwa Kutumia Bruda
Bruda ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahusus kwa ajili ya kuwapatia
joto vifaranga badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga
wengi kwa kutumia bruda ambayo ni mduara unaweza kutengenezwa kwa
kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa kuziba pembe za chumba.Aidha,
njia hii hupunguza vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na ndege au
wanyama hatari,huruhusu kuku kutaga mapema zaidi na kuwa na
mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). Vilevile, hurahisisha
udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa
kutumia bruda:-
• Kuweka vifaa vya kuongeza joto kwa mfano taa ya umeme, chemli au
jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto kinachohitajika katika bruda.
Wiki ya kwanza ni 35oc, wiki ya pili ni 33oc, wiki ya tatu ni 31oc na
wiki ya nne ni 29oc,
• Kuchunguza mtawanyiko wa vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini
hali ya joto.Wakijikusanya kwenye chanzo cha joto, inaashiria kuwa
baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa mbali na chanzo cha joto
maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
• Bruda iwe na sakafu yenye malalo yatokanayo na maranda ya mbao
au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe endapo yataonekana
yameloana,
• Bruda iwekwe vifaa vya maji na chakula. Maji na chakula kiwekwe
kabla ya kuweka vifaranga,
• Vifaa vya joto viwekwe ndani ya bruda masaa 6 kabla ya kuingiza
vifaranga,
• Vifaranga walishwe chakula cha kuanzia gramu 12-15 kwa kipindi
cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21-35 kwa kifaranga
na chakula hicho kiwepo muda wote,
• Vifaranga wapatiwe vitamin, madini na dawa za kinga (antibiotics); na
• Vifaranga wapatiwe chanjo kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa
mifugo.Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu kwa mfano,Marek’s (mara
anapototolewa), Mdondo (siku ya 3-4 na kurudiwa baada ya siku ya
21 na kila baada ya miezi 3) na Gumboro (siku ya 7na kurudia tena
siku ya 21).Wapatiwa dawa ya minyoo (wiki ya 8) na coccidiosis(wiki
ya 3-4). Siku ya 45 wapewe chanjo ya ndui ya kuku.
2. Kutunza Kuku Wanaokua (Wiki 8-18)
Utunzaji wa kundi hili unategemea mfumo unaotumika.
Kuku Wanaofugwa Katika Mfumo Huria
Kuku wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora
yakiwemo yafuatayo;
• Wapewe chakula cha ziada asubuhi kabla ya kutoka na
wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza kugawanywa
mara ya 2 kwa siku,
• Wapatiwe maji safi na ya kutosha wakati wote
• Wapatiwe chanjo na dawa kulingana na ushauri wa mtaalam wa
mifugo. Wiki ya kumi warudie chanjo ya mdondo, wiki ya 12
kuhara (fowl cholera), wiki ya 14 ndui ya kuku,
Kuku Wanaofugwa Katika Mfumo Shadidi
• Majogoo watenganishwe na mitetea katika wiki 7 hadi 10 ili
kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
• Wapewe chakula cha kukuzia kuanzia wiki ya 8-15 gramu 55-
60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65-80 kwa wanaofugwa mfumo
huria na gram 120-125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa
mfumo wa shadidi,
• Kuku wa nyama wapatiwe chakula cha kuku wa nyama muda
wote,
• Wapatiwe maji safi ya kunywa kwa muda wote kwenye
vyombo safi,
• Kuku wachunguzwe dalili zozote za ugonjwa ili waweze kupata
tiba sahihi kutoka kwa mtalaamu wa mifugo,
• Kuku wa wiki 9-20 wanahitaji nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa
kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa kuku,
• Kuwe na vyombo maalum vya kutosha kwa ajili ya chakula na
maji,
• Wafanyiwe usafi wa banda mara kwa mara ili kuzuia magonjwa
yanayotokana na uchafu
• Wakatwe midomo ili kuzuia kudonoana.
3. Kuku Wanaotaga
Mahitaji ya kuku wanaotaga ni tofauti na makundi mengine.
Mambo ya kuzingatia kwa kuku wanaotaga ni pamoja na:-
• Banda liwe na viota vya kutagia mayai (kiota 1 kwa kuku 3-
5).Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha umri wa
wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
• Wapatiwe chakula na maji safi wakati wote kwa kutumia
vyombo maalum ambavyo ni visafi,
• Kuku wasiotaga waondolewe kwenye kundi.Kuku hao
huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na
kavu,upanga wake kichwa (comb) huwa mdogo na
mwekundu,
• Wapatiwe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3,
• Wawekewe fito au ubao mwembamba kama sehemu ya
kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
• Mayai yakusanywe mara 4 au zaidi kwa siku ili yasidonolewe
na kuku,
• Kuwe na malalo makavu na yabadilishwe mara yanapochafuka,
• Vyombo vifanyiwe usafi kila ili kuzuia magonjwa; na
• Watundikiwe majani mabichi aina ya mchicha,papai,
alfaafa,majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe.
Udhibiti na Tiba Dhidi ya Magonjwa ya Kuku
Kuku wanaopata lishe bora, kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo
dhidi ya magonjwa yanayotokea mara kwa mara huwa na afya nzuri.
Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama.
Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe na kuku
wasio wagonjwa na wapatiwe tiba. Kanuni muhimu za kufuata ili
kuzuia magonjwa ni:-
• Banda liwe safi muda wote,
• Kabla ya kuweka kuku, banda linyunyuziwe dawa ya kuua
wadau wa magonjwa mbalimbali,
• Kuku wakaguliwe kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye
matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
• Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,
• Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
• Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,
• Banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo
mingine,
• Lango la kuingia katika banda la kuku liwekewe dawa ya
kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea
vya wadudu wa magonjwa;na
• Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote.
Dalili za Kuku Mgonjwa
Dalili za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama
zifuatazo:-
• Kuzubaa,
• Kupoteza hamu ya kula,
• Kujitenga na wenzake katika kundi; na
• Kupunguza au kusimama kutaga.
UFUGAJI WA SAMAKI: MABWAWA YA KUFUGIA SAMAKI
Bwawa hili limejengwa pia kwa simenti kutoka usawa wa ardhi kwenda juu, ni la mduara kama linavyoonekana kwenye picha hii. Yapo mabwawa mengi ya aina hii katka kituo cha kufugia samaki Kingolwira mjini Morogoro. |
Ufugaji wa samaki unamanufaa sana kwa mfugaji kwani unaweza kumuondolea Mtanzania umaskini huku akiendelea kujipatia kitoweo.
UFUGAJI WA NG'OMBE
Ng'ombe wa kienyeji ndiyo wanaofugwa kwa wingi Tanzania bara na Visiwani ikiwa ni asilimia 96.2 bara na asilimia 95.2 visiwani. Ng'ombe wa nyama na maziwa walioboreshwa ni asilimia (0.9 na 2.9) kwa bara na asilimia (0.7 na 4.1) kwa visiwani. Idadi ya ng'ombe Tanzania bara na visiwani inaonekana kupongezeka ukilinganisha na ya sensa ya mwaka 2002/2003 kwa ng'ombe 4,281,082. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa mkoa wa Shinyanga ndio unaofuga ng'ombe wengi zaidi ikifuatiwa na Tabora. Mikoa mingine inayofuga ng'ombe wengi kuanzia milioni moja hadi mbili ni Mwanza, Arusha, Mara, Manyara, Singida and Dodoma
Chanzo: (Repoti ya taifa iliyotolewa mwezi wa tatu mwaka huu inayotokana na sensa iliyofanyika mwaka 2007/2008 kwa kutumia sampuli).
No comments:
Post a Comment